Sunday, January 19, 2014

Kasi ya kutekeleza matokeo makubwa sasa katika elimu "BIG RESULT NOW" Tanzania


   Home
 
   
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo P. Pinda amesema maisha ya Watanzania yatabadilika na kuwa bora zaidi kama kila kiongozi atawajibika na kutekeleza kilichoahidiwa na Serikali katika Dira ya Taifa ya Maendeleo na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
 
Mhe. Pinda aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo kuhusu Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na Mpango wa Maendeleo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Dodoma ambayo kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni, 2013.
 
Alisema ili kuleta maendeleo, ushirikiano kutoka katika ngazi mbalimbali zikiwepo Sekta binafsi, Taasisi za Serikali, Taasisi zisizo za Kiserikali pamoja na wananchi wa kawaida kuwa ni muhimu katika kutekeleza Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaojulikana kama “ Matokeo Makubwa Sasa ” ili kuondokana na taratibu za “Kufanya kwa Mazoea” na kuanza kufanya kazi katika utaratibu wa “ Kufanya Mambo Isivyo Kawaida”.
 
Alisema mfumo mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo unaojulikana kama Matokeo Makubwa Sasa unajikita katika kuchambua kwa kina programu na miradi ya kipaumbele iliyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao umelenga katika kuainisha maeneo machache yatakayoweza kuleta matokeo makubwa kwa haraka.
 
Alizitaja Sekta Sita ambazo zimepewa kipaumbele katika mfumo wa Matokeo Makubwa sasa kuwa ni Maji, Nishati, Usafirishaji, Elimu, Kilimo na Mapato.
 
“Tumeanza na vipaumbele hivi kwasababu vinabeba msingi wa kufungulia fursa ya mapinduzi ya kiuchumi katika maeneo mengine ya kiuchumi na vinaathiri moja kwa moja katika hali ya kiuchumi na kijamii kwa Mtanzania mmoja mmoja “ Alisema Mhe. Pinda na kuongeza kwamba uteuzi wa Sekta hizi umezingatia umuhimu wake kwani vimebeba msingi wa kufungulia fursa ya Mapinduzi ya Kiuchumi katika maeneo mengine kiuchumi na kwamba vinaathari ya moja kwa moja katika hali ya kiuchumi na kijamii kwa Mtanzania mmoja mmoja ili kuleta ustawi wa pamoja nchini.
 
 
 
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi Mhe. Mizengo P. Pinda waliokaa kulia kwake ni Waziri wa Nchi OWM – TAMISEMI Mhe. Hawa A. Ghasia (MB) na Prof. Jumanne Maghembe Waziri wa Maji (MB) nje ya Ukumbi wa Dodoma Hoteli, Mjini Dodoma.
 
Naye Waziri wa Nchi-TAMISEMI Mhe. Hawa Ghasia akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo alisema mafunzo hayo yanalenga katika kutoa fursa ya kuwaelimisha washiriki katika maeneo yanayohusu utaratibu mpya wa utendaji, usimamizi na kupima matokeo unaojulikana kama “Tekeleza Sasa Kwa Matokeo Makubwa ” yaani “Big Results Now”
 
“ Ni imani yangu kwamba mafunzo haya yatawapa uelewa wa kina kuhusu mfumo huu wa “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa ” Alisema Mhe. Ghasia.
 
Chimbuko la mfumo huu wa Matokeo Makubwa sasa umetokana na maamuzi yaliyochukuliwa na Serikali ya kutumia mfumo mpya kutokana na Mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo ilibainika kwamba kuna kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi, programu na mikakati ya maendeleo na baada ya mapitio ya Dira yameonyesha kuwa kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
 
Katika mfumo huu, viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Watendaji katika Mikoa na Idara watapimwa kwa vigezo vilivyo wazi ambapo wananchi watapata fursa ya kuvijua vigezo hivi pamoja na matokeo ya upimaji na hatimaye mwisho wa siku ufanisi wa viongozi utapimwa kwa kutumia vigezo vilivyokubaliwa tokea mwanzo.
 
Ili kuratibu vyema shughuli za ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mfumo huu mpya kimeundwa chombo maalum kitakachokuwa chini ya Ofisi ya Rais kinachojulikana kama ”Presidential Delivery Bureau” (PDB) ambacho kitakuwa ndiyo nyenzo ya kumwezesha Mhe. Rais kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa katika Mpango wa Maendeleo miaka Mitano na Dira ya Taifa ya 2025 yanafikiwa.
 
Hotuba ya Waziri Mkuu - Mh. Mizengo Pinda
Hotuba ya Waziri wa Nchi - Mh. Hawa Ghasia
 

No comments: