Saturday, August 15, 2015

Yafahamu Madhara ya Ulaji wa Chumvi kupita kiasi Mwilini

CHUMVI ni dawa ya mboga.” Watu wengi hupenda kusema hivyo. Tangu enzi na enzi, chumvi ni miongoni mwa viungo muhimu vya chakula. Mbali na kuwa na madhara inapotumiwa vibaya, lakini bado ni muhimu kwa mwili wa binadamu. Chumvi ni aina ya madini yenye umuhimu na faida nyingi kwa mtumiaji akama atatumiwa kwa kiasi kinachotakiwa kitaalamu kwenye mlo wake. Kimsingi, chumvi si rahisi kuikosa kwenye nyumba zetu. Hupatikana kirahisi kwa kuwa bei yake ni nafuu, ikikilinganishwa na viungo vingine vya jikoni. Wataalamu na wanasayansi wanasema kwamba matumizi ya chumvi kupita kiasi, ni kichocheo cha magonjwa ya moyo, yanayochangia vifo vingi vya watu duniani kwa sasa. Ingawa watu wengi wanaichukulia chumvi kama kiungo cha kawaida tu kisichokuwa na umuhimu mkubwa, lakini inapaswa kufahamika kuwa kiungo hicho kina umuhimu mkubwa katika afya ya mwanadamu. Ukweli ni kwamba chumvi ni madini yanayosaidia kuhifadhi maji mwilini, kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, kusaidia tezi ambazo kitaalamu zinaitwa Thyroid, na zaidi husaidia katika suala zima la upatikanaji wa usingizi. Wataalamu wa afya wanashauri utumiaji mzuri wa chumvi katika vyakula, kwa kuwa inapotumika vibaya, huwa inasababisha madhara mbalimbali kwenye mwili wa mwanadamu. Utafiti uliofanyika Machi, 2013, kabla ya kuwasilishwa katika mkutano wa Chama cha Wenye Matatizo ya Moyo mjini, New OrleĆ”ns, Marekani, ulibainisha kuwa matumizi ya chumvi kupita kiasi kulichangia vifo vilivyohusiana na matatizo ya moyo kiasi cha takriban watu milioni 2.3 duniani kote. Kwa mujibu wa Radio Tehran ya Iran, asilimia 42 ya watu hao walikufa kutokana na magonjwa ya moyo, wakati asilimia 41 walifariki dunia kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Hii ni kwa mujibu wa vifo vilivyorekodiwa mwaka 2010 pekee. Idadi hii inajumuisha walaji wa chumvi nyingi iliyomo kwenye vyakula vingi vya makopo na maboksi, ambavyo hutumia chumvi zenye kiwango kingi cha Sodium inayoongezwa wakati wa kutengenezwa kwa vyakula hivyo viwandani. Katika utafiti huo, iligundulika kuwa nchi inayoongoza kwa watu wake kula chumvi nyingi kuliko nchi zote duniani, ni Kazakhstan iliyoko Asia ya Kati, jirani na nchi ya Urusi. Kwa mujibu wa utafiti huo, kwa wastani Wakazakhstan hula kiasi cha miligramu 6,000 za chumvi ambayo ni zaidi ya vijiko vidogo vitatu kila siku moja. Katika ripoti ya utafiti huo, nchi za Kenya na Malawi ndizo zenye kiwango kidogo zaidi cha matumizi ya chumvi duniani, kwa wastani wa miligramu 2,000. Wastani wa kiwango cha chumvi kinachokubalika kiafya, ambao mtu anatakiwa kula kwa siku ni miligram 2,300 tu. Hii ni sawa na kijiko kidogo cha chumvi kwa siku nzima. Inapozidi kiwango hicho mwilini, chumvi hiyo husababisha matatizo mengine ya kiafya. Lazima tuzingatie hili. Wataalamu wa afya wamekaririwa wakisema kwa watu wale wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu, wanatakiwa kutozidisha kiasi cha miligramu 1,500 kwa siku. Wapo wanaopinga kipimo hiki wakidai kwamba watu wanaochuruzikwa na jasho kupita kiasi, wanaofanya kazi za sulubu, wanamichezo na wanaoishi katika nchi za joto, wanatakiwa kula chumvi zaidi. Hata hivyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Phili Chilo, anasema: “Chumvi ikitumiwa vibaya husababisha maradhi ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. “Baadhi ya magonjwa hayo ni pamoja na moyo kushindwa kusukuma damu, kutanuka na mengineyo yanayoweza kusababisha mtu apatwe na mshituko wa ghafla wa moyo na kupoteza maisha.” Hali hiyo inachangiwa pia na matumizi yasiyo sahihi ya chumvi. Ili kuepuka maradhi hayo, jamii inashauriwa kuwa na tabia ya kupima afya. Kwa hiyo, ni vema kutumia kiwango kinachohitajika cha chumvi wakati wa kupika chakula kwa kuwa chumvi mbichi ya kuongezea mezani, si nzuri kiafya, inapaswa kuepukwa. Wananchi wanashauriwa pia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya chumvi kwenye vyakula. Aidha, kwa wale wanaopenda kula vyakula vya makopo na vifungashio vingine, wanashauriwa kusoma maelekezo ili kufahamu kiasi cha chumvi iliyomo kwenye vyakula hivyo. Madhara ya chumvi mwilini Kuna matatizo makubwa mawili kwenye ulaji wa chumvi ambayo hufanya chumvi kuwa hatari. Mosi, ni watu kuzidisha kiwango cha chumvi kwa kuweka chumvi nyingi kwenye vyakula vyao au kununua vyakula vilivyokwisha kutengenezwa na kuwekwa chumvi nyingi. Pili, kula chumvi isiyo sahihi, kwa maana ya chumvi inayopatikana kiasili na si kwa kutengenezwa. Ili kupata faida ya chumvi iliyokusudiwa, ni lazima siku zote tutumie ile ambayo haijatengenezwa na kuongezewa kemikali nyingine zenye madhara kwa mwili. Chumvi asilia huwa na virutubisho muhimu ambavyo madini ya Sodium na Chloride, ambavyo huingia mwilini kwa kula lishe sahihi. Kwa bahati mbaya sana, chumvi inayotumiwa na watu wengi haina madini hayo ya kutosha, kutokana na kutengenezwa upya viwandani kwa kusafishwa (Refined). Kwa mujibu wa maelezo ya Taasisi ya Maradhi ya Shinikizo la Moyo ya Uingereza, chumvi ikizidi mwilini husababisha maradhi ya moyo, saratani ya tumbo, matatizo ya figo, ubongo kuwa msahaulifu uzeeni, maradhi ya mifupa, pumu na kadhalika. Madhara mengine kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni kwamba kutodhibiti ulaji wa chumvi, huchangia ongezeko la vifo na maradhi kama vile kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, mshituko wa moyo, na macho kupoteza uwezo wa kuona na kadhalika. Faida ya chumvi mwilini Utumiaji sahihi wa chumvi na kwa kiwango kinachotakiwa, una faida nyingi mwilini. Faida hizo ni pamoja na kuimarisha na kudhibiti shinikizo la damu, kuboresha ufanisi wa misuli ya mwili, kuboresha ufanisi wa ubongo na kadhalika. “Chumvi ikitumiwa kwa kiasi kinachotakiwa, haina madhara mwilini. Chumvi ikitumiwa vizuri, ni dawa mwilini. Lakini ikitumiwa vibaya, huleta madhara makubwa ya kiafya kwa walaji pasipo wao kufahamu,” anasema mmoja wa wataalam wa mambo ya vyakula na kuongeza. “Lakini, ili kupata faida hizo, ni lazima chumvi yenyewe iwe ni ya asilia ambayo haijachakachuliwa wala kuongezwa kemikali nyinginezo. Kwa maana nyingine, ulaji wa chumvi iliyoondolewa madini yake muhimu na kuongezwa kemikali nyingine pamoja na kula kupita kiwango cha kawaida, husababisha chumvi kuwa na madhara badala ya faida mwilini, hivyo kugeuka na kuwa chanzo cha matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Kwa hali hiyo, kila mtu hana budi kupunguza matumizi ya chumvi, kutumia chumvi asilia muda wote, kwa maana ya chumvi inayochimbwa na kuuzwa kienyeji ambayo ni bora zaidi kuliko ile inayopitia viwandani ambapo huondolewa Sodium na Chloride, na wakati mwingine huongezwa kemikali nyingine hatari zaidi. Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema ulaji mkubwa wa chumvi unatakiwa kupunguzwa kama ambavyo uvutaji sigara unavyotakiwa. Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kwamba mabara ya Afrika na Asia, yamefanikiwa kuzingatia ushauri wa kupunguza matumizi ya chumvi zaidi ikilinganishwa na mabara mengine ulimwenguni. Kwa mujibu wa tafiti hizo, hali hiyo ya mabara ya Afrika na Asia kufanikiwa kuzingatia ushauri wa kupunguza ulaji wa chumvi, imeweza kuzuia vifo vya takriban watu 92,000 kwa mwaka katika mabara hayo, vifo ambavyo vingetokana na ulaji mwingi wa chumvi. Kwa mfano, utafiti uliofanywa mwaka 2012 na Dk Derin Balogun anayeongoza kampeni ya kuzuia maradhi ya moyo na shinikizo la damu duniani, ulibainisha kwamba, hoteli nyingi za Waafrika na watu weusi jijini London, Uingereza, hupika vyakula vyenye chumvi nyingi zaidi. Kwa mujibu wa Dk. Balogun, gramu 12 zilipatikana katika wali na maharagwe, gramu 8.6 ndani ya wali maarufu kwa jina la 'Jollof' kutoka Afrika Magharibi, wakati gramu 19 iligundulika kwenye mikate. Hii ni chumvi zaidi ya gramu tano, zinazotakiwa kwa mtu mzima kutumia kila siku. Si vibaya ukifahamu kwamba chumvi ya asili hupatikana pia ndani ya vyakula vya asili vyenye madini ya Sodium kama vile mayai, nyama na hata baadhi ya vyakula vinavyotokana na maziwa. Mayai kwa mfano, yana miligramu 30 za Sodium. Kwa wale wanaopendelea kula vyakula vinavyopikwa nje ya nyumba zao, kama vile katika hoteli na kwenye migahawa, wanapaswa kuwa waangalifu mno kwa kuwa vyakula vya ‘fast food’ ni vyenye kiwango kikubwa cha chumvi na mafuta pia. Vyakula kama vile chizi, soseji, sosi ya soya na achari mbalimbali ni vyenye kutengenezwa kwa kutumia kiwango kikubwa cha chumvi. Lakini pia chumvi hutumiwa katika kuhifadhi baadhi ya vyakula vya makopo na maboksi. Elimu kama hii ya faida na madhara ya chumvi ni muhimu kwa Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuipatia kipaumbele kwa kutoa kwa wananchi wake, kwa faida ya taifa na watu wake. Ipo haja kwa jamii nzima ya Watanzania kuelimishwa vya kutosha kuhusu faida na madhara ya chumvi katika mwili mwa mwanadamu kuliko ilivyo sasa ambapo wananchi wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu ulaji wa chumvi.

Yafahamu Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, Chanzo chake na jinsi Kuishi nayo

Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa ni magonjwa yanayoathiri njia za hewa pamoja na sehemu nyingine zinazohusiana na mapafu, kama vile magonjwa ya Pumu, Kufungana kwa njia za pumzi (Chronic Obstructive Pulmonary Disease-COPD), ugonjwa wa mapafu unaotokana na kazi (Occupational Lung Disease), kupanda kwa shinikizo la damu kwenye Mapafu (Pulmonary Hypertension) na kadhalika. Magonjwa haya, mara nyingi huathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa hewa na kuzuia kiasi cha hewa inayotoka na kuingia kwenye mapafu, kwa mfano ugonjwa wa Pumu. Hali hii humfanya mgonjwa apumue au kuvuta hewa kwa shida, hasa pale anapokuwa mgonjwa. Magonjwa haya huweza kusababisha kuwepo kwa makohozi katika njia ya hewa, hivyo kusababisha maambukizi mengine. Kutokana na Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 235 duniani kote wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa Pumu, huku watu milioni 64 wakitajwa kusumbuliwa na magonjwa sugu ya kufungamana kwa njia ya Pumzi (COPD). Kwa mujibu wa WHO, takriban asilimia 90 ya vifo vinavyotoakana na magonjwa hayo, hutokea katika nchi zilizo na uchumi duni na wa kati, Tanzania ikiwa mojawapo. Watu wengi hudhani kwamba mtu anapokuwa mwembamba kupita kiasi na akawa na uzito kidogo, basi mtu huyo atakuwa na ugonjwa wa Ukimwi. Wanaodhani hivyo, hawajui kwamba magonjwa sugu ya njia ya hewa, nayo yanaweza kumsababishia mtu akakonda na kupungua uzito pia. Hali hiyo hutokea kutokana na ukweli kuwa magonjwa hayo ya njia ya hewa, humfanya mgonjwa atumie nguvu nyingi wakati wa kupumua kuliko mtu asiyekuwa na magonjwa hayo. Matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kupumua, humfanya mgonjwa asiwe na nishati ya akiba ambayo huhifadhiwa mwilini, hivyo kufanya mtu kuwa mnene. Lakini pia unene uliokithiri, unaweza kusababisha magonjwa mugu ya njia ya hewa. Ni nini chanzo cha magonjwa sugu ya njia ya hewa? Magonjwa Sugu ya Njia ya Hewa, mara nyingi husababishwa na kuharibika kwa njia ya hewa katika mapafu. Uharibifu huo wa njia ya hewa huweza kutokana na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugolo; kuvuta hewa yenye sumu au vumbi kutoka viwandani, uchafuzi wa hewa ya ndani mfano kwa kutumia jiko la utambi na mafuta ya taa; uchafuzi wa hewa ya nje kutokana na vumbi au poleni ya maua na unene uliokithiri kiwango. Anayesumbuliwa na ugonjwa sugu wa njia ya hewa azingatie nini ili aweze kuishi? Mgonjwa wa ugonjwa sugu wa njia ya hewa anashauriwa kuzingatia ushauri wa daktari na matibabu yake, kufuata kanuni za mtindo bora wa maisha, kuepuka visababishi kama vile vumbi, barafu na harufu, kuhakikisha mazingira na nyumba anaoishi ni safi muda wote, na zaidi pia iwe na madirisha yanayoruhusu mzunguko wa hewa. Aidha, wagonjwa wa magonjwa hayo wanashauriwa kula mlo kamili na vyakula vya aina mbalimbali ili wapate virutubishi vyote vinavyohitajika kwa afya zao. Inashauriwa kula zaidi matunda freshi, mbogamboga zenye rangi ya kijani, matunda yenye rangi ya njano kama vile ndizi, papai, embe, mapera na kadhalika. Lakini pia, wanashauriwa kula vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi ili kusaidia mfumo wa kusaga chakula kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa uchafu tumboni kwa urahisi. Hali hii huwasaidia kuweza kupumua kwa urahisi. Ikumbukwe kuwa mgonjwa wa aina hiyo anatumia nguvu nyingi wakati wa kupumua, hivyo basi anahitaji kula chakula cha kutosha ili kumpatia nguvu za kutosha. Ni vizuri kula milo midogo midogo mara kwa mara, ikiwa ni pamoja nakupunguza matumizi ya chumvi ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kusababisha kupumua kwa shida. Ni muhimu pia kuepuka uzito uliozidi kwa sababu unene huongeza tatizo la kupumua. Je, mgonjwa wa mugonjwa sugu wa njia ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi? Mazoezi ya mwili yana faida nyingi kiafya. Baadhi ya faida hizo ni kuimarisha mapafu na moyo. Ili kuviwezesha viungo hivyo muhimu katika mwili wa mwanadamu vifanye kazi kwa ufanisi, mazoezi ni muhimu sana. Aidha, mazoezi husaidia kuimarisha misuli ambayo hutumika wakati wa kupumua. Kwa hiyo, mgonjwa wa magonjwa sugu ya hewa anaruhusiwa kufanya mazoezi kwa sababu mazoezi ni sehemu ya matibabu yake. Mgonjwa anapaswa kujitahidi mara kwa mara kufanya mazoezi, kwa kuanza mazoezi ya taratibu kwa kadri mwili wake unavyoweza kustahimili, na kisha kuongeza hatua kwa hatua. Hata hivyo, inashauriwa mgonjwa anayefanya mazoezi, pindi asikiapo maumivu kifuani au kushindwa kuhimili mazoezi hayo, punguza kasi ya mazoezi hayo na fanya kwa taratibu kadri iwezekanavyo.

HATARI: Vimelea vipya vya Kisonono Visivyotibika kama Virusi vya Ukimwi vyagundulika

WAKATI dunia ikipalangana kutafuta dawa ya kutibu ugonjwa wa Ukimwi, imeripotiwa kubainika kwa vimelea vipya vya ugonjwa wa Kisonono, ambavyo havisikii dawa za ugonjwa huo zilizokuwa zimezoeleka ulimwenguni kama tiba sahihi ya maradhi hayo, hivyo ugonjwa huo sasa sasa kutajwa kuwa hatari sawa na Ukimwi. Taarifa mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inaeleza kwamba kuna aina mpya vimelea vya ugonjwa wa kisonono vinavyoendelea kusambaa kwa kasi duniani, ambavyo vinahimili dawa zilizokuwa zinatumika kutibu ugonjwa bila kudhulika. Kwa mujibu wa WHO, vimelea hivyo vipya havisikii dawa, hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma, zimekuwa hazina tena athari kwa vijidudu vipya hivyo. Tayari nchi nyingi duniani zimeripotiwa kukumbwa na usungu wa kisonono hata pale mgonjwa anapopatiwa tiba sahihi ya Antibiotiki (Viuasumu) za jamii ya Sefalosporini na kadhalika, zikiwemo Hongkong, Australia, Ufaransa, Japan, Norway, Sweden na Uingereza. Aina hii mpya ya vimelea vya kisonono vinadaiwa kuonyesha usugu dhidi ya dawa zote za Antibiotiki zinazotumiwa kuviangamiza, zikiwemo dawa hizo za jamii ya Sefalosporini, ambazo WHO inazitaja kama dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono. Dk. Manjula Lusti-Narasimhan, kutoka Kitengo cha Afya ya Uzazi na Utafiti cha WHO, amekaririwa akisema: “Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya Antibiotiki (Viuavijasumu) jamii ya Sefalosporini viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway." Daktari huyo hakukomea hapo, bali anasema katika miaka michache ijayo, aina hii mpya ya vimelea vya ugonjwa wa kisonono, huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo zinapatikana kwa sasa ulimwenguni. Dk. Manjula anasema: “Ugonjwa sugu wa kisonono si tatizo la Bara la Ulaya au Afrika pekee, bali ni tatizo la dunia nzima. Lazima tahadhari zichukuliwe mapema. Upo uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa kwa haraka duniani kote bila kugundulika. Hii inatokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake.” Baadhi ya Wanasayansi wa magonjwa hayo ya zinaaa wanaamini kwamba matumizi holela ya dawa aina ya Antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa huo kubadilika na kuzoea mazingira mapya, ndicho chanzo kikuu cha ugonjwa huo kwa sasa kuwa sugu. Kwa mujibu wa wanasansi hao, ugonjwa wa kisonono ambacho si sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (Cervix), Urethra na Puru, hutibiwa kwa Antibiotiki (Kiuavijasumu) jamii ya Sefalosporini, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya Macrolide kama vile Azithromycin, na za jamii ya Penicillin kama vile Doxycyclin kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Chlamydia. Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano. Mgonjwa lazima afuate masharti na ushauri wa daktari kabla hajatumia dawa hizo, kwa kuwa dawa nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano Doxycyclin. “Kawaida ushauri nasaha hutolewa kwa washirika wote wawili wa ngono. Na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama mmoja wao hatakuwa na dalili za ugonjwa huu wa kisonono,” wanasema Watafiti na Wanasayansi kuhusu tiba sahihi ya ugonjwa huo. Namna ya kujikinga na ugonjwa huo mpya wa kisonono Utafiti wa wanasayansi waliobobea katika magonjwa ya binadamu, wanasema kwamba mtu anaweza kujikinga na ugonjwa wa kisonono kwa kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha vitendo vya zinaa na uasherati. Aidha, mtu anaweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo kwa mshirika wake wa ngono pindi mmoja wapo anapojibaini kuwa na hali yenye dalili zote za ugonjwa ili wote kwa pamoja waweze kutibiwa na kupata ushauri wa daktari mapema. Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono au kujenga tabia ya kutumia mipira ya kiume (Kondomu) wakati wa kujamiiana. Kwa upande wa wanawake wajawazito ni muhimu kuhudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa huo wa zinaa au ugonjwa mwingine wowote. Kwa mujibu wa WHO, wanawake wajawazito wanatakiwa wajifungulie katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ili kama watoto wanaozaliwa watabainika kuathirika kwa ugonjwa huo wa kisonono waweze kupata matibabu ya mapema mara tu baada ya kuzaliwa hivyo kuwaepusha na uwezekano wa kupata upofu. Kutokana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo mpya wa kisonono, kila nchi duniani, kupitia Serikali zao na madaktari wao, zinapaswa kuongeza umakini katika ufuatiliaji wa aina hii mpya ya ugonjwa wa kisonono kwa sababu ugonjwa huo una madhara makubwa kwa afya ya binadamu kama vile kusababisha ugumba kwa wanawake, utasa kwa wanaume, upofu, moyo, uvimbe, ubongo na homa ya mapafu. Takwimu zilizopo kutoka WHO, zinaonyesha kwamba kisonono ni ugonjwa hatari kwa usalama wa binadamu, hivyo muda si mrefu ugonjwa huo unaweza kutangazwa kama moja ya majanga makubwa ya dunia, kama hatua madhubuti na haraka hazitachukuliwa kwa kila nchi. Kutokana na hali hiyo, WHO imezitaka nchi zote duniani kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake, pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za Antibiotiki hadi pale taarifa kamili za ugonjwa huo zitakapojulikana. SambazaTweet about this on Twitter2Share on Facebook8Share on Google+0Share on LinkedIn0Email this to someonePrint this page

Dalili za Ugonjwa wa Uvimbe wa Tezi za Uzazi kwa Wanawake na Tiba yake

Wanawake wengi wanavyoteseka na tatizo la kutoshika ujauzito bila ya kujua sababu yake pia ni nini. Moja ya sababu ya kutoshika ujauzito, ni ugonjwa wa Sisti au Nziba unaopatikana kwenye Ovari za uzazi (Ovarian Cyst). Katika makala haya ya sehemu ya pili tutaangazia tena dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa huu wa Sisti/Nziba. Dalili na viashiria vya kwanza kabisa vya ugonjwa wa Sisti/Nziba kwenye Tezi za Uzazi za Mwanamke ni maumivu makali ambayo hayana mwanzo maalum na yanayochoma, ambapo maumivu hayo yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja. Lakini pia, mwanamke anaweza kupata usumbufu na kutojisikia vizuri kwenye maeneo ya chini ya kitovu, kwenye nyonga, uke, kwenye mapaja na mgongoni upande wa chini kiunoni. Dalili nyingine ni maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati mwanamke anapokuwa kwenye siku zake, maumivu ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya kiunoni. Kwa kawaida mumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi. Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu, mazoezi au baada ya kujamiiana. Kuhisi kichefuchefu, kutapika na kutokwa na matone ya damu ukeni. Ugumba na kuhisi uchovu, mabadiliko ya haja ndogo, yaani kukojoa mara kwa mara, kujikojolea au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo. Mabadiliko ya haja kubwa, kwa maana ya kupata haja kubwa kwa shida sana kutokana na presha kwenye maeneo ya nyonga; nywele kukua kwa kasi na kuongezeka kuota kwa nywele kwenye uso au sehemu nyingine za mwili. kuumwa kichwa, kuongezeka uzito, maumivu ya kwenye mbavu, kutokewa na uvimbe chini ya ngozi na kuvimba mara kwa mara; maumivu kwenye matiti na kuapata hedhi isiyokuwa na mpangilio maalumu na kuhisi tumbo kuwa zito, kujaa au kuvimba. Mwanamke mwenye dalili na viashiria hivi afanye nini? Kwanza kabisa ni kufanyiwa kipimo cha mawimbi ya sauti ndani ya uke (Endovaginal Ultrasound). ambacho hufanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke. Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama kuna uvimbe wowote kwenye Ovari na uvimbe huo ni wa aina gani au atajua kama ni maji tu (Fluid filled sac), au ni maji pamoja na mchanganyiko wa ute mzito, au ni ute mzito pekee. Kipimo kingine kinachoweza kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi ni kipimo cha mawimbi ya sauti kutoka kwenye nyonga hadi kwenye fumbatio (Pelvic Abdominal Ultrasound) ambayo ni Ultrasound ya kawaida. Hii husaidia kujua aina ya uvimbe uliopo kwenye tezi za uzazi (Ovari) za mwanamke. Vipimo vingine vinavyoweza kuonyesha uvimbe kwenye Ovari ni pamoja na Computerized Tomography (CT) Scan na Magnetic Resonance Imaging (MRI) Scan. Matibabu ya Ugonjwa wa Tezi za Uzazi za Mwanamke Matibabu ya Sisti/Nziba kwenye Ovari yanategemea sana umri, aina na ukubwa wa uvimbe pamoja na dalili anazohisi mgonjwa. Mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ili kupunguza hatari ya kupata Sisti/Nziba kwenye Ovari. Ni muhimu kufahamu kwamba vidonge vya uzazi wa mpango, mbali na kuzuia upatikanaji wa mimba zisizokuwa na mpango, hupunguza pia hatari ya kupata Kansa au Saratani kwenye Ovari za Uzazi wa Mwanamke. Kwa hiyo, matiba ya magonjwa haya yanaweza kuhusisha vipimo vya damu kama CA-125 ili kuangalia uvimbe huo kama ni Saratani au ni uvimbe wa kawaida tu. Uvimbe kama haupungui na unasababisha maumivu makali sana, mgonjwa anaweza kushauriwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo. Kama mgonjwa atalazimika kufanyiwa upasuaji, uvimbe uliotolewa unaweza kupelekwa kwa mtaalam wa Patholojia kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kupata bainisho la mwisho la ugonjwa (Final Diagnosis). Endapo uchunguzi utaonyesha kwamba uvimbe huo ni wa Saratani, basi Daktari atamshauri mgonjwa kutolewa kwa viungo vyote vya uzazi (Total Hysterectomy) ili kuzuia Saratani kutosambaa kwenye viungo vingine. SambazaTweet about this on Twitter0Share on Facebook5Share on Google+0Share on LinkedIn0Email this to someone

Wanaotoa Mimba chini ya Miaka 18, hatarini kupata Ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi

WASICHANA wanaopata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18 pamoja na wenye tabia ya kutoa mimba mara kwa mara, wametajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi. Mbali na kundi hilo, pia watumiaji wa dawa za kulevya, watu wenye magonjwa ya zinaa, wanawake wanaozaa mara kwa mara na wanaume wasio tahiriwa nao wapo katika hatari ya kupata aina hiyo ya saratani. Mshauri wa masuala ya Afya ya Uzazi, Leojin Mnzava, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibaha, amebainisha hayo katika mafunzo ya kuwapatia elimu hiyo ya Afya ya Uzazi wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wilayani humo na kuwa tayari wameanza kutoa elimu ya ugonjwa wa Saratani ya shingo ya kizazi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanafunzi walio na tabia ya kufanya mapenzi kabla ya wakati. Amesema kwamba saratani ya shingo ya kizazi, ni hatari kuliko magonjwa mengine kama vile Ukimwi na Malaria, hivyo wanawake wanapaswa kuwa makini na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha au kuchochea magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa huo. Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Asasi ya Maendeleo ya Wanawake ya INUKA, Gaudience Msuya, yenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam, amesema wametoa mafunzo kwa walimu 40 waliopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, ambayo yamelenga kuwakumbusha walimu visababishi vya saratani ya shingo ya kizazi ili waielimishe jamii wakiwemo wanafunzi. Lindi yatajwa kuongoza Saratani za Matiti na Shingo ya kizazi Wakati huo huo, Mkoa wa Lindi umetajwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake waliogundulika kuwa na saratani ya matiti na shingo ya kizazi kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutambua dalili za ugonjwa huo, ambao kama ukitambuliwa mapema unatibika. Daktari Faridi Ally kutoka Hospitali ya Sokoine iliyoko Mkoani Lindi, amebainisha hayo wakati wa mahojiano na FikraPevu na kwamba wataalamu kutoka katika hospitali hiyo wamekwishaanza kutoa elimu kwa wanawake zaidi ya 300, juu ya kutambua dalili za ugonjwa wa saratani na kusisitiza umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo. Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza, amesema mipango ya Serikali ya mkoa ni pamoja na kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo na kwamba kwa kuanza wameanza kutoa elimu ili kupunguza tatizo kabla ya mipango hiyo haijakamilika. Saratani ya kizazi ni nini? Ni aina ya saratani inayoshambulia seli/chembechembe zilizoko kwenye ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi. Chanzo cha ugonjwa huo ni kirusi kiitwacho 'Human Pailloma Virus' na huambukizwa kwa njia ya kujamiana na mtu mwenye maambukizi hayo. Aidha, dalili za ugonjwa ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na majimaji au uchafu usio wa kawaida ukeni, kutokwa na damu ukeni wakati ambao mwanamke hayuko kwenye hedhi pamoja na maumivu makali wakati wa kujamiana. Tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi za Afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) zimebainisha kwamba tabia hatarishi inayopelekea kupata magonjwa haya ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 18), uvutaji wa sigara, kuzaa mara kwa mara, matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula, kuwa na wapenzi wengi au kujamiana na mtu mwenye wapenzi wengi.

Unataka kutumia Vidonge vya Uzazi wa Mpango Kuzuia Mimba? Jiandae na Madhara 10 haya

Vidonge vya Uzazi wa Mpango, ni moja ya njia inayopendekezwa na Wataalamu wa Mpango wa Uzazi katika kuzuia mimba. Hata hivyo, vidonge hivyo vinaweza kutimiza malengo hayo ya mpango huo ikiwa tu vitatumiwa vizuri na kwa usahihi, kwa sababu tafiti zilizopo, zinaonyesha kwamba asilimia nane (8%) ya wanawake hupata mimba zisitarajiwa kila mwaka, huku wakiwa katika mpango huo kutokana na baadhi yao kujisahau kumeza vidonge hivyo. Kwa mujibu wa tafiti, vidonge hivyo vya mpango wa uzazi vikitumiwa vizuri, kwa kuhakikisha muda wa matumizi yake unakuwa ule ule, ni mwanamke mmoja pekee kati ya 100 anayeweza kupata mimba isiyotarajiwa ndani ya mwaka wa kwanza wa matumizi ya dawa hizo. Hadi sasa kuna aina kuu mbili tu za vidonge vya uzazi vinavyotumiwa na wanawake katika wa mpango huo, ingawa aina zote hizo zina vichocheo (hormons). Aina hizo kitaalamu zinaitwa Estrogen na Progesteron. Estrogen ni aina ya kichocheo kinachotengenezwa na uterasi/kizazi, kinachosaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi, kwa kuongoza ukuaji wa kuta za uterasi kwenye sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi. Kwa upande wake, Progesteron, hiki ni kichocheo cha kopasi luteamu ya ovari, kinachosaidia kuanzisha mabadiliko katika endometriumu baada ya ovulesheni. Ingawa katika aina hiyo mbili ya vidonge, kuna vingine vina kichocheo cha aina moja tu, kwa maana ya ama Estrogen au Progestron, huku vingine vikiwa na vichocheo vyote viwili hivyo, lakini vidonge vyote hivyo ni salama, na vinafanya kazi kwa kufanya ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na kuzuia kupevuka kwa yai, hivyo kuzuia mimba kwa kiwango cha asilimia 99. Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza pia kutumika kama tiba ya kuweka sawa mzunguko wa hedhi, kuzuia maumivu makali wakati wa hedhi, kutibu chunusi pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa katika via vya uzazi, ambayo hayatokani au kusababishwa na magonjwa ya ngono. Hata hivyo, pamoja na usalama wa vidonge hivyo katika kufanya kazi yake hiyo ya kuzuia mimba na tiba kwa magonjwa hayo, vidogo hivyo vinaweza kumsababishia athari za kiafya mwanamke kama havitumiki katika mpangilio sahihi. Athari kuu 10 zinazoweza kusababishwa na vidonge hivyo ni pamoja na kutokwa na damu ukeni baada ya hedhi ya kawaida. Kwa mujibu wa wataalam wa mpango huo, athari hiyo huweza kuwapata asilimia 50 ya wanawake wote wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango. Hali hii huweza kuwatokea ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza matumizi ya dawa hizi. Kwa ujumla, hali hiyo huweza kukoma kwa zaidi ya asilimia 90, pindi mwanamke anapoanza kutumia pakti ya tatu ya dawa hizo katika kipindi hicho cha kutokwa damu ukeni. Mwanamke anapotokewa na hali hiyo kwa mfululizo wa siku tano au zaidi baada ya kumaliza siku zake za kawaida za hedhi, anashauriwa kuwasiliana na mhudumu wa afya wakati akiendelea kutumia dawa hizo. Athari ya pili, ni kujisikia kichefuchefu. Mara nyingi hali hiihumtokea mwanamke mwanzoni tu baada ya kuanza kumeza vidonge vya uzazi wa mpango, ingawa hali hii inaweza kukoma baada ya siku chache. Inashauriwa pia kwa mwanamke anayepatwa na hali hii ya kichefuchefu kuwasiliana na mhudumu wa afya kama ataona hali hiyo inazidi. Matiti kujaa au kuwa na maumivu, ni athari nyingine inayoweza kusababisha na matumizi ya vidonge hivyo. Hali hii huweza kumpata baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo, na huweza kukoma ndani ya wiki moja tu. Hata hivyo, inashauriwa kwamba ikiwa matiti hayo yatatokwa na uvimbe au maumivu yasiyoisha, ni muhimu kutafuta tiba kwa wahudumu wa afya, ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya kinywaji chenye kafeini na chumvi na kuvaa brauzi isiyobana matiti. Maumivu ya kichwa ni athari nyingine inayoweza kumtokea mwanamke, ingawa pia kuumwa kichwa kunaweza kuwa na dalili za magonjwa mengine. Hata hivyo, kama itatokea maumivu hayo ya kichwa yakaanza tu mara baada ya kumeza vidonge hivyo, hiyo itakuwa ni dalili ya athari mojawapo na ni vyema kutoa taarifa kwa mhudumu wa afya. Vidonge vua uzazi wa mpango huweza pia kuongezeka uzito wa mtumiaji, ingawa tafiti nyingine zimeshindwa kuthibitisha uhusiano kati ya vidonge hivyo na mabadiliko ya uzito wa mtumiaji. Aidha, baadhi ya wanawake hupatwa na tatizo la maji kuganda kwenye matiti na maeneo ya nyonga baada ya kutumia vidonge hivyo. Mabadiliko ya hisia huweza pia kumtokea mwanamke anayeanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Inashauri kwamba pindi mwanamke anapoona dalili hii, ni muhimu kumjulisha mhudumu wa afya ili kuweza kujadili ni jinsi gani ataweza kutumia dawa hizo, kwa sababu dalili hii ni mbaya kiafya kwa mtu mwenye historia ya ugonjwa wa Kushuka Moyo (Depression). Adhari nyingine ya dawa hizi ni kutokwa na uchafu ukeni. Baadhi ya wanawake, mara tu baada ya kutumia vidonge hivi hutokwa na uchafu ukeni, ikiwa ni pamoja na kupatwa na uwezekano wa kupungua au kuzidi kwa ute wakati wa tendo la ndoa. Ni muhimu sana mwanamke anapobaini dalili hizi, kuonana na mhudumu wa afya ili kubaini kama hali hiyo imesababishwa na athari ya vidonge au kuna maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Wanawake wengine huweza kujikuta wakikosa siku zao za hedhi baada ya kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Ingawa ugonjwa wa msongo wa mawazo (Stress), magonjwa, mchoko wa safari unaweza kusababisha hali hii, lakini inashauriwa kupima kama mtu amaepatwa na ujauzito hata kama anatumia vidonge hivi kama itatokea kukosa hedha katika mazingira tata. Kupungua kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa ni athari nyingine inayoweza kumkuta mwanamke anayetumia vidonge vya uzazi wa mpango kutokana na vichocheo vilivyomo ndani ya dawa hizo, ingawa pia magonjwa kama ya kisukari, shinikizo kubwa la damu na kadhalika yanaweza pia kuchangia tatizo hilo. Athari ya 10 na ya mwisho kwa wanawake wanaotumia vidonge hivyo, ni mabadiliko ya taswira ya kitu anachokiona mbele yake, hasa kwa wanawake wanaovaa miwani ya macho. Kwa kuwa macho ni moja ya eneo muhimu la ufahamu kwa mwanadamu, hali hii inapowapata wanawake, inashauri kuonana mara moja na daktari wa macho pindi tu dalili hizi zinapoanza kujitokeza. Ni tahadhari gani mwanamke anatakiwa kuchukua kabla na baada ya kuanza matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango? Kwa mwanamke mzazi, hairuhusiwi hata kidogo kuanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ndani ya wiki tatu tu baada ya kujifungua mtoto au ikiwa atakuwa ananyonyesha mtoto mwenye umri wa chini ya miezi sita. Aidha, ikiwa mwanamke amefanyiwa upasuaji mkubwa wa aina yoyote katika siku za karibuni, au kama mwanamke husika ni mvutaji wa sigara na ana umri wa zaidi ya miaka 35, haruhusiwi kutumia vidonge hivyo, kama ambavyo pia haruhusiwi kufanya hivyo mwanamke mwenye historia ya ugonjwa wa ini, manjano, moyo, saratani ya matiti, tumbo la uzazi pamoja na shinikizo la damu linalobadilikabadilika kila wakati kwa viwango vya 140/90 au zaidi, na au kama ana historia ya maumivu makali ya kichwa.

Madhara ya Heroin kwa wajawazito

WAKALA wa maabara ya mkemia wa serikali, ndiyo mamlaka yenye jukumu hapa nchini ya kufanya uchunguzi wa kitaalam ili kubaini, kutambua na kuthibitisha aina na madhara ya dawa za kulevya. Mamlaka hiyo inaeleza kuwa, Heoin ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaojulikana kama Oppium poppy. Kilimo cha mmea huo hufanyika kwa kiwango kikubwa katika nchi ya Afghanistani. Vile vile mmea huo unalimwa kidogo nchini Misri. Dawa hii hupambaza mfumo wa fahamu na kusababisha mtu kupata usingizi, kupungua kwa mawazo na maumivu makali. Majina mengine ya Heroin ni Unga, Brown Sugar, Ngoma, ubuyu, Mondo, Dume, Farasi na Ponda. Kwa mujibu wa kijarida cha wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, idara ya huduma za sayansi ya makosa ya jinai(Forensic Science Services), kinaainisha madhara wayapatayo wajawazito wanaotumia dawa aina hii. Madahara hayo kwa wajawazito ni pamoja na upungufu wa damu mwilini, mimba kuharibika, kujifungua watoto njiti, kujifungua watoto ambao hufariki kabla ya kutimiza miaka mitano na watoto kupata matatizo ya kiafya ikiwemo kuchelewa kukua kiakili. Mengini ni kuleta mabadiliko ya hedhi kwa wanawake na hujenga hali ya uteja kwa haraka sana kuliko dawa zingine za kulevya. Madhara ya kijamii Madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa za kulevya kwa jamii ni pamoja na kuvunjika kwa ndoa, kutoweka kwa amani katika jamii ikiwemo ongezeko la fujo na uhalifu, matatizo ya mwajiri na mwajiliwa na ongezeko la mzigo kwa jamii na vyombo vya usalama na taifa kwa ujumla. Madhara ya jumla kwa watumiaji wa dawa hii ni kuharibika kwa mfumo wa fahamu, kapata njozi, kupata magonjwa ya moyo, ini, kifua kikuu na kupumjua, kushuka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu. Kwa watumiaji wa Heroin kwa njia ya kujidunga wanapata matatizo ya kuambukizana VVU kwa kuwa baadhi yao hushirikiana sindano, kuzubaa na kupunguza uwezo wa kufanya kazi, kichefuchefu, kizunguzungu na dozi kubwa hupelekea kifo.

Yafahamu madhara ya Mirungi

MIRUNGI ni aina ya mimea inayostawi kwenye hali ya unevunyevu na milima yenye urefu wa kati ya futi 4000 hadi 9000. Hapa nchini mimea hii hupatikana kwa wingi kama uoto wa asili katika mikoa ya Arusha, Kilimajaro, Manyara na Tanga. Hata hivyo kiasi kikubwa cha mirungi itumikayo nchini huingizwa isivyo halali kutoka nchini Kenya. Mirungu hujulikana kwa majina mengi kama vile Miraa, Mbaga, Mogoka, Veve, Bomba na Kashamba. Kwa mujibu wa wakala wa Maabara ya mkemia Mkuu wa Seriali ya Tanzania, Mirungi ina kemikali inayojulikana kama “Cathinone”, ambayo mtumiaji akitumia hukosa hamu ya kula. Madhara mengine kwa mtumiji wa Mirungi ni kutokwa na vidonda vya mdomoni na tumboni, kukosa choo, kupungukiwa maji mwilini, kupata shinikizo la damu, kupungukiwa nguvu za kiume, mwili kuwasha, kupata maumivu makali ya kichwa na kuharibika ini. Sheria ya dawa za kulevya ya mwaka 1995, inasema kuwa, ni kosa la jinai, kutumia, kuhamasisha matumizi, kuhifadhi au kujihusisha kwa namna yeyote ile na mirungi.

Cocain na madhara kwa mtumiaji na jinsi ya kumsaidia

COCAINE ni dawa ya kulevya inayotengenezwa kutokana na mmea wa coca, unaostawishwa katika nchi za Amerika ya kusini. Dawa hii ipo katika kundi la kichangamshi kikali ambacho huathiri mfumo wa ufahamu. Cocaine huwa katika unga mweupe au katika hali yam awe madogo madogo. Majina ya mtaani Cocaine hujulikana kwa majina mengi ikiwemo; Unga, White sugar, Keki, Big C, Bazooka, Snow, Keki, Unga mweupe nk. Kinachotokea baada ya kutumia Cocaine. Kwa mujibu wa kijarida kilichotolewa na ofisi ya wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali na kupatikana katika banda la Tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya nchini, katika maazimisho ya kupinga dawa za kulevya kitaifa yaliyofanyika Jijini Mbeya June 26, mwaka huu kinaeleza. Kijarida hicho kinaeleza kuwa, wenyeji wa Amerika ya kusini, hutumia cocaine kwa kutafuna. Aidha, unga mweupe wa cocaine, hutumika kwa njia ya kuvuta kwa kutumia pua au kunusa. Cocaine aina yam awe madogo madogo hutumika kwa njia ya kuvuta. Mara baada ya kutumia cocaine kwa kiwango kidogo, dalili zifuatazo zinaweza kuonekana. Dalili hizo kwa mtumiaji ni uchangamfu kupita kiasi, kupungua kwa hamu ya chakula, kupanuka kwa mboni za macho, kukauka koo, kutokutulia, kuwa na mhemuko wa kufanya ngono, kusinyaa kwa mishipa ya damu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu. Jukumu la maabara ya mkemia mkuu wa serikali Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, unalo jukumu la kufanya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini, kutambua na kuthibitisha aina na madhara ya dawa za kulevya Madhara yatokanayo na matmizi ya kiwango kikubwa cha cocaine. Madhara hayo ni pamoja na njozi/maono yasiyokuwepo, kuchanganyikiwa, kuwashwa mwili, kuwa na hasira za ghafla, hisia za kuwepo vijidudu mwilini, kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo kunakoweza kusababisha kiharusi au kifo, kuongezeka na kupungua kwa mapigo ya moyo ghafla na kutetemeka kwa nguvu kama kifafa. Meneja wa mafunzo kutoka shirika la kifaransa la MDM, lenye makao makuu wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, linaloshughulika na upunguzaji wa athari zitokanazo na matmizi y dawa za kulevya, Damal Lucas, anasema kuwa, cocain inachangamsha mfumo wa fahamu lakini huisha haraka mwilini. Damali anasema dawa hiyo ikiisha katika mwili wa mtumiaji, inasababisha mtumiaji kujisikia vibaya(Alosto) ikiwemo kukosa raha, kusonaneka na kunyongea. Ili kuzuia hali hii, watumiaji wengi huendelea kutimia. Dawa hii ni hatari sana na huleta utegemezi katika kipindi cha muda mfupi baada ya utumiwa. Mtumiaji huweza kuiba,kutapeli, kudanganya na hata kuwa jambazi ili kupata fedha za kununulia dawa hii. Madhara mengine ni mtumiaji kupata madhara ya kisaikolojia yanayoweza kufanya kuwa mkorofi, mkali na mwenye fujo, kukosa ufanisi kazini na kupata matatizo ya kifamilia. Madhara mengine ya kiafya ni kutokwa damu puani, kutokwa na vidonda puani, magonjwa ya ini, kuziba mishipa ya damu, kuharibika mishipa ya fahamu, mchafuko wa damu na kupata majipu na kuharibika kwa moyo na figo. Kama cocaine ikitumika kwa kuvuta au kunusa mfumo wa upumuaji huathirika na kumfanya mtumiaji kushindwa kupumua vizuri, kikohozi cha muda mrefu, maumivu ya kifua na kuharibika kwa mapafu. Matumizi ya cocaine na dawa zingine za kulevya humweka mtumiaji katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU na huongeza uwezekano wa kifo cha mapema. Utamsaidiaje mtumiaji wa cocaine? Kama mmojawapo wa marafiki au mtu wako wa karibu anatumia cocaine, mwambie ukweli kuwa cocaine huathiri ubongo, mwili na hisia zake. Vile vile ajue kwamba anaweza kuwa mtegemezi wa dawa hii na kusababisha kifo. Mwonyeshe unamjali.

BANGI INAVYOINGIZWA KATIKA MAGEREZA

BANGI ni dawa ya kulevya iliyopo kwenye kundi la dawa za kulevya lenye kuleta Njozi (Hellucinogences). Vileta njozi huathiri ubongo na kumfanya mtumiaji kutoa tafsiri potofu ya hisia na kujisikia kama vile yuko nje ya dunia. Mtumiaji wa bangi huzalishwa na kutumiwa kwa wingi barani Afrika kwa sababu hustawi maeneo mengi. Nchini Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini, mkoani Njombe wilayani Makete hustawi zaidi. Wakati Serikali ikiamini kuwa gerezani ni mahala salama hata kuwatunza wanaokamatwa na dawa za kulevya, hali si shwari katika baadhi ya magereza hapa nchini, kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa hizo. Baadhi ya askari Magereza, wafungwa na mahabusu katika magereza mbalimbali hapa nchini, wanahusishwa na biashara ya dawa za kulevya ndani ya magereza, imebainika. Uchunguzi uliofanywa kwa miezi miwili sasa, umebaini kuwepo kwa dawa za kulevya katika magereza mengi hapa nchini, hususani Bangi. Baadhi ya askari ambao hawakutaka kutajwa majina yao na vyeo katika Gereza la Ruanda na Songwe mkoani Mbeya, walithibitisha kuwepo kwa uingizwaji wa bidhaa hiyo ambayo inafanyika kwa siri kubwa katika magereza hayo. Biashara hiyo inahusisha baadhi ya askari, wafungwa na mahabusu wenye kesi mbalimbali, wanaokaa muda mrefu gerezani huku kesi zao zikiahirishwa mara kwa mara. Baadhi ya waliowahi kuwa mahabusu wa gereza la Ruanda mkoani Mbeya, wanaeleza kuwa wahusika wakubwa ni baadhi ya wafungwa wanaofanya kazi nje ya gereza, kisha kurejeshwa alasiri na baadhi wanaopelekwa mahakamani kusomewa mashitaka ya kesi zinazowakabili. Wanasema njia ambazo zinatumika kuingiza dawa hizo gerezani ni kujiingiza katika sehemu ya haja kubwa wakiwa nje ya gereza na wakati wa ukaguzi unapofanyika kwa kila anayeingia gerezani hapo, askari wanashindwa kubaini. “Baadhi ya wafungwa ambao wanakaribia kumaliza muda wao, wanatolewa kwenda kufanya kazi za nje ikiwemo kwenda kukata nyasi za Ng’ombe na kurejeshwa mchana na wale wanaoenda kusaga mashine wanaweka kwenye unga. Hao wana mtandao na wauza bangi uraiani, wanaingia nazo na kufanya biashara ndani ya gereza, mle kuna biashara nyingi” anaeleza mmoja wa aliyekuwa mahabusu katika gereza hilo na kuachiliwa huru hivi karibuni baada ya Mahakama kuona hana hatia. Baadhi ya askari mgambo wanaotumwa kuwachukua mahabusu na kuwapeleka katika mahakama za mwanzo, ambao nao waliomba hifadhi ya majina yao, walikiri kuwepo kwa biashara hiyo ambapo walisema kuwa, biashara hiyo inafanyika kutokana na vipato vidogo vya Mgambo na askari Magereza kutokuwa na mianya ya rushwa tofauti na askari polisi. Mbali na bangi, wanasema kuwa, katika magereza pia kuna uvutaji mkubwa wa sigala ambazo huingizwa kwa njia za haja kubwa kisha kutolewa vyooni na kuhifadhiwa katika maeneo mbalimbali ya sero na nje ya sero bustanini. Wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali, idara ya huduma za sayansi ya makosa ya jinai (GCRLA), inataja madhara yanayowakuta watu wanaotumia dawa hii ya kulevya kuwa ni kuwaza, kuona, kusikia na kuhisi vitu kwa namna tofauti au visivyokuwepo, kupata njozi, kuongezeka kwa hamu ya kula, kuwa kama kichaa, kutapika, wasiwasi, hamaki na kupumbaa. Madhara yatokanayo na matumizi ya muda mrefu Madhara hayo ni kupata ugonjwa wa akili, mabadiliko ya maono, hisia na mtizamo yasiyoisha, kuharibika kwa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kukumbuka na kufikiri na kukosa ari ya maendeleo na mabadiliko ya aina yoyote ile. Sheria inasemaje kuhusu bangi Kutumia, kuhamasisha matumizi, kuuza, kusafirisha, kuhifdhi au kujihusisha kwa namna yeyote ile na bangi ni kosa la jinai. Adhabu kwa makosa haya hufikia hadi kifungo cha maisha. Sheria inasemaje kuhusu bangi Kutumia, kuhamasisha matumizi, kuuza, kusafirisha, kuhifdhi au kujihusisha kwa namna yeyote ile na bangi ni kosa la jinai. Adhabu kwa makosa haya hufikia hadi kifungo cha maisha. Mbali na tatizo la Bangi, moja ya matatizo yanayotajwa ni suala la kutumia kwa kubadilishana vitu vyenye ncha kali zikiwemo nyembe. “Nilikamatwa na kupelekwa gerezani mwaka 2011, nikakuta watu wananyolea wembe mmoja ambapo kilichoniuma ni kwamba kuna rafiki yangu aitwaye Jack, alikuwa anaishi na VVU, alinyolea wembe akajikata, akampa jamaa anaitwa Kamugisha akajikata, naye akampa Side, naye akajikata na Side alimpa Chidi akatie kucha naye akajikata, virusi vikasambaa kwa wote”anasema Frank Kaitaba, kijana ambaye alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam na sasa anahudumiwa na shirika la Medecin De Munde la Temekelinalopunguza athari za madawa ya kulevya.. Anasema baada ya hapo akaamua kuwafuata madaktari wa gereza hilo na kuanzisha kikundi cha uelimishaji rika ndani ya gereza na kwamba tangu hapo ndani ya gereza hilo mtu anapotaka kunyoa anampa taarifa kiongozi aitwaye Onyango, ambaye anatoa wembe na kumwamuru nyapala asimamie matumizi ya nyembe.