Saturday, August 15, 2015

Cocain na madhara kwa mtumiaji na jinsi ya kumsaidia

COCAINE ni dawa ya kulevya inayotengenezwa kutokana na mmea wa coca, unaostawishwa katika nchi za Amerika ya kusini. Dawa hii ipo katika kundi la kichangamshi kikali ambacho huathiri mfumo wa ufahamu. Cocaine huwa katika unga mweupe au katika hali yam awe madogo madogo. Majina ya mtaani Cocaine hujulikana kwa majina mengi ikiwemo; Unga, White sugar, Keki, Big C, Bazooka, Snow, Keki, Unga mweupe nk. Kinachotokea baada ya kutumia Cocaine. Kwa mujibu wa kijarida kilichotolewa na ofisi ya wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali na kupatikana katika banda la Tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya nchini, katika maazimisho ya kupinga dawa za kulevya kitaifa yaliyofanyika Jijini Mbeya June 26, mwaka huu kinaeleza. Kijarida hicho kinaeleza kuwa, wenyeji wa Amerika ya kusini, hutumia cocaine kwa kutafuna. Aidha, unga mweupe wa cocaine, hutumika kwa njia ya kuvuta kwa kutumia pua au kunusa. Cocaine aina yam awe madogo madogo hutumika kwa njia ya kuvuta. Mara baada ya kutumia cocaine kwa kiwango kidogo, dalili zifuatazo zinaweza kuonekana. Dalili hizo kwa mtumiaji ni uchangamfu kupita kiasi, kupungua kwa hamu ya chakula, kupanuka kwa mboni za macho, kukauka koo, kutokutulia, kuwa na mhemuko wa kufanya ngono, kusinyaa kwa mishipa ya damu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu. Jukumu la maabara ya mkemia mkuu wa serikali Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, unalo jukumu la kufanya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini, kutambua na kuthibitisha aina na madhara ya dawa za kulevya Madhara yatokanayo na matmizi ya kiwango kikubwa cha cocaine. Madhara hayo ni pamoja na njozi/maono yasiyokuwepo, kuchanganyikiwa, kuwashwa mwili, kuwa na hasira za ghafla, hisia za kuwepo vijidudu mwilini, kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo kunakoweza kusababisha kiharusi au kifo, kuongezeka na kupungua kwa mapigo ya moyo ghafla na kutetemeka kwa nguvu kama kifafa. Meneja wa mafunzo kutoka shirika la kifaransa la MDM, lenye makao makuu wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, linaloshughulika na upunguzaji wa athari zitokanazo na matmizi y dawa za kulevya, Damal Lucas, anasema kuwa, cocain inachangamsha mfumo wa fahamu lakini huisha haraka mwilini. Damali anasema dawa hiyo ikiisha katika mwili wa mtumiaji, inasababisha mtumiaji kujisikia vibaya(Alosto) ikiwemo kukosa raha, kusonaneka na kunyongea. Ili kuzuia hali hii, watumiaji wengi huendelea kutimia. Dawa hii ni hatari sana na huleta utegemezi katika kipindi cha muda mfupi baada ya utumiwa. Mtumiaji huweza kuiba,kutapeli, kudanganya na hata kuwa jambazi ili kupata fedha za kununulia dawa hii. Madhara mengine ni mtumiaji kupata madhara ya kisaikolojia yanayoweza kufanya kuwa mkorofi, mkali na mwenye fujo, kukosa ufanisi kazini na kupata matatizo ya kifamilia. Madhara mengine ya kiafya ni kutokwa damu puani, kutokwa na vidonda puani, magonjwa ya ini, kuziba mishipa ya damu, kuharibika mishipa ya fahamu, mchafuko wa damu na kupata majipu na kuharibika kwa moyo na figo. Kama cocaine ikitumika kwa kuvuta au kunusa mfumo wa upumuaji huathirika na kumfanya mtumiaji kushindwa kupumua vizuri, kikohozi cha muda mrefu, maumivu ya kifua na kuharibika kwa mapafu. Matumizi ya cocaine na dawa zingine za kulevya humweka mtumiaji katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU na huongeza uwezekano wa kifo cha mapema. Utamsaidiaje mtumiaji wa cocaine? Kama mmojawapo wa marafiki au mtu wako wa karibu anatumia cocaine, mwambie ukweli kuwa cocaine huathiri ubongo, mwili na hisia zake. Vile vile ajue kwamba anaweza kuwa mtegemezi wa dawa hii na kusababisha kifo. Mwonyeshe unamjali.

No comments: