Saturday, August 15, 2015

Madhara ya Heroin kwa wajawazito

WAKALA wa maabara ya mkemia wa serikali, ndiyo mamlaka yenye jukumu hapa nchini ya kufanya uchunguzi wa kitaalam ili kubaini, kutambua na kuthibitisha aina na madhara ya dawa za kulevya. Mamlaka hiyo inaeleza kuwa, Heoin ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaojulikana kama Oppium poppy. Kilimo cha mmea huo hufanyika kwa kiwango kikubwa katika nchi ya Afghanistani. Vile vile mmea huo unalimwa kidogo nchini Misri. Dawa hii hupambaza mfumo wa fahamu na kusababisha mtu kupata usingizi, kupungua kwa mawazo na maumivu makali. Majina mengine ya Heroin ni Unga, Brown Sugar, Ngoma, ubuyu, Mondo, Dume, Farasi na Ponda. Kwa mujibu wa kijarida cha wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, idara ya huduma za sayansi ya makosa ya jinai(Forensic Science Services), kinaainisha madhara wayapatayo wajawazito wanaotumia dawa aina hii. Madahara hayo kwa wajawazito ni pamoja na upungufu wa damu mwilini, mimba kuharibika, kujifungua watoto njiti, kujifungua watoto ambao hufariki kabla ya kutimiza miaka mitano na watoto kupata matatizo ya kiafya ikiwemo kuchelewa kukua kiakili. Mengini ni kuleta mabadiliko ya hedhi kwa wanawake na hujenga hali ya uteja kwa haraka sana kuliko dawa zingine za kulevya. Madhara ya kijamii Madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa za kulevya kwa jamii ni pamoja na kuvunjika kwa ndoa, kutoweka kwa amani katika jamii ikiwemo ongezeko la fujo na uhalifu, matatizo ya mwajiri na mwajiliwa na ongezeko la mzigo kwa jamii na vyombo vya usalama na taifa kwa ujumla. Madhara ya jumla kwa watumiaji wa dawa hii ni kuharibika kwa mfumo wa fahamu, kapata njozi, kupata magonjwa ya moyo, ini, kifua kikuu na kupumjua, kushuka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu. Kwa watumiaji wa Heroin kwa njia ya kujidunga wanapata matatizo ya kuambukizana VVU kwa kuwa baadhi yao hushirikiana sindano, kuzubaa na kupunguza uwezo wa kufanya kazi, kichefuchefu, kizunguzungu na dozi kubwa hupelekea kifo.

No comments: