Saturday, August 15, 2015

Yafahamu Madhara ya Ulaji wa Chumvi kupita kiasi Mwilini

CHUMVI ni dawa ya mboga.” Watu wengi hupenda kusema hivyo. Tangu enzi na enzi, chumvi ni miongoni mwa viungo muhimu vya chakula. Mbali na kuwa na madhara inapotumiwa vibaya, lakini bado ni muhimu kwa mwili wa binadamu. Chumvi ni aina ya madini yenye umuhimu na faida nyingi kwa mtumiaji akama atatumiwa kwa kiasi kinachotakiwa kitaalamu kwenye mlo wake. Kimsingi, chumvi si rahisi kuikosa kwenye nyumba zetu. Hupatikana kirahisi kwa kuwa bei yake ni nafuu, ikikilinganishwa na viungo vingine vya jikoni. Wataalamu na wanasayansi wanasema kwamba matumizi ya chumvi kupita kiasi, ni kichocheo cha magonjwa ya moyo, yanayochangia vifo vingi vya watu duniani kwa sasa. Ingawa watu wengi wanaichukulia chumvi kama kiungo cha kawaida tu kisichokuwa na umuhimu mkubwa, lakini inapaswa kufahamika kuwa kiungo hicho kina umuhimu mkubwa katika afya ya mwanadamu. Ukweli ni kwamba chumvi ni madini yanayosaidia kuhifadhi maji mwilini, kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, kusaidia tezi ambazo kitaalamu zinaitwa Thyroid, na zaidi husaidia katika suala zima la upatikanaji wa usingizi. Wataalamu wa afya wanashauri utumiaji mzuri wa chumvi katika vyakula, kwa kuwa inapotumika vibaya, huwa inasababisha madhara mbalimbali kwenye mwili wa mwanadamu. Utafiti uliofanyika Machi, 2013, kabla ya kuwasilishwa katika mkutano wa Chama cha Wenye Matatizo ya Moyo mjini, New Orleáns, Marekani, ulibainisha kuwa matumizi ya chumvi kupita kiasi kulichangia vifo vilivyohusiana na matatizo ya moyo kiasi cha takriban watu milioni 2.3 duniani kote. Kwa mujibu wa Radio Tehran ya Iran, asilimia 42 ya watu hao walikufa kutokana na magonjwa ya moyo, wakati asilimia 41 walifariki dunia kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Hii ni kwa mujibu wa vifo vilivyorekodiwa mwaka 2010 pekee. Idadi hii inajumuisha walaji wa chumvi nyingi iliyomo kwenye vyakula vingi vya makopo na maboksi, ambavyo hutumia chumvi zenye kiwango kingi cha Sodium inayoongezwa wakati wa kutengenezwa kwa vyakula hivyo viwandani. Katika utafiti huo, iligundulika kuwa nchi inayoongoza kwa watu wake kula chumvi nyingi kuliko nchi zote duniani, ni Kazakhstan iliyoko Asia ya Kati, jirani na nchi ya Urusi. Kwa mujibu wa utafiti huo, kwa wastani Wakazakhstan hula kiasi cha miligramu 6,000 za chumvi ambayo ni zaidi ya vijiko vidogo vitatu kila siku moja. Katika ripoti ya utafiti huo, nchi za Kenya na Malawi ndizo zenye kiwango kidogo zaidi cha matumizi ya chumvi duniani, kwa wastani wa miligramu 2,000. Wastani wa kiwango cha chumvi kinachokubalika kiafya, ambao mtu anatakiwa kula kwa siku ni miligram 2,300 tu. Hii ni sawa na kijiko kidogo cha chumvi kwa siku nzima. Inapozidi kiwango hicho mwilini, chumvi hiyo husababisha matatizo mengine ya kiafya. Lazima tuzingatie hili. Wataalamu wa afya wamekaririwa wakisema kwa watu wale wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu, wanatakiwa kutozidisha kiasi cha miligramu 1,500 kwa siku. Wapo wanaopinga kipimo hiki wakidai kwamba watu wanaochuruzikwa na jasho kupita kiasi, wanaofanya kazi za sulubu, wanamichezo na wanaoishi katika nchi za joto, wanatakiwa kula chumvi zaidi. Hata hivyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Phili Chilo, anasema: “Chumvi ikitumiwa vibaya husababisha maradhi ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. “Baadhi ya magonjwa hayo ni pamoja na moyo kushindwa kusukuma damu, kutanuka na mengineyo yanayoweza kusababisha mtu apatwe na mshituko wa ghafla wa moyo na kupoteza maisha.” Hali hiyo inachangiwa pia na matumizi yasiyo sahihi ya chumvi. Ili kuepuka maradhi hayo, jamii inashauriwa kuwa na tabia ya kupima afya. Kwa hiyo, ni vema kutumia kiwango kinachohitajika cha chumvi wakati wa kupika chakula kwa kuwa chumvi mbichi ya kuongezea mezani, si nzuri kiafya, inapaswa kuepukwa. Wananchi wanashauriwa pia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya chumvi kwenye vyakula. Aidha, kwa wale wanaopenda kula vyakula vya makopo na vifungashio vingine, wanashauriwa kusoma maelekezo ili kufahamu kiasi cha chumvi iliyomo kwenye vyakula hivyo. Madhara ya chumvi mwilini Kuna matatizo makubwa mawili kwenye ulaji wa chumvi ambayo hufanya chumvi kuwa hatari. Mosi, ni watu kuzidisha kiwango cha chumvi kwa kuweka chumvi nyingi kwenye vyakula vyao au kununua vyakula vilivyokwisha kutengenezwa na kuwekwa chumvi nyingi. Pili, kula chumvi isiyo sahihi, kwa maana ya chumvi inayopatikana kiasili na si kwa kutengenezwa. Ili kupata faida ya chumvi iliyokusudiwa, ni lazima siku zote tutumie ile ambayo haijatengenezwa na kuongezewa kemikali nyingine zenye madhara kwa mwili. Chumvi asilia huwa na virutubisho muhimu ambavyo madini ya Sodium na Chloride, ambavyo huingia mwilini kwa kula lishe sahihi. Kwa bahati mbaya sana, chumvi inayotumiwa na watu wengi haina madini hayo ya kutosha, kutokana na kutengenezwa upya viwandani kwa kusafishwa (Refined). Kwa mujibu wa maelezo ya Taasisi ya Maradhi ya Shinikizo la Moyo ya Uingereza, chumvi ikizidi mwilini husababisha maradhi ya moyo, saratani ya tumbo, matatizo ya figo, ubongo kuwa msahaulifu uzeeni, maradhi ya mifupa, pumu na kadhalika. Madhara mengine kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni kwamba kutodhibiti ulaji wa chumvi, huchangia ongezeko la vifo na maradhi kama vile kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, mshituko wa moyo, na macho kupoteza uwezo wa kuona na kadhalika. Faida ya chumvi mwilini Utumiaji sahihi wa chumvi na kwa kiwango kinachotakiwa, una faida nyingi mwilini. Faida hizo ni pamoja na kuimarisha na kudhibiti shinikizo la damu, kuboresha ufanisi wa misuli ya mwili, kuboresha ufanisi wa ubongo na kadhalika. “Chumvi ikitumiwa kwa kiasi kinachotakiwa, haina madhara mwilini. Chumvi ikitumiwa vizuri, ni dawa mwilini. Lakini ikitumiwa vibaya, huleta madhara makubwa ya kiafya kwa walaji pasipo wao kufahamu,” anasema mmoja wa wataalam wa mambo ya vyakula na kuongeza. “Lakini, ili kupata faida hizo, ni lazima chumvi yenyewe iwe ni ya asilia ambayo haijachakachuliwa wala kuongezwa kemikali nyinginezo. Kwa maana nyingine, ulaji wa chumvi iliyoondolewa madini yake muhimu na kuongezwa kemikali nyingine pamoja na kula kupita kiwango cha kawaida, husababisha chumvi kuwa na madhara badala ya faida mwilini, hivyo kugeuka na kuwa chanzo cha matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Kwa hali hiyo, kila mtu hana budi kupunguza matumizi ya chumvi, kutumia chumvi asilia muda wote, kwa maana ya chumvi inayochimbwa na kuuzwa kienyeji ambayo ni bora zaidi kuliko ile inayopitia viwandani ambapo huondolewa Sodium na Chloride, na wakati mwingine huongezwa kemikali nyingine hatari zaidi. Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema ulaji mkubwa wa chumvi unatakiwa kupunguzwa kama ambavyo uvutaji sigara unavyotakiwa. Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kwamba mabara ya Afrika na Asia, yamefanikiwa kuzingatia ushauri wa kupunguza matumizi ya chumvi zaidi ikilinganishwa na mabara mengine ulimwenguni. Kwa mujibu wa tafiti hizo, hali hiyo ya mabara ya Afrika na Asia kufanikiwa kuzingatia ushauri wa kupunguza ulaji wa chumvi, imeweza kuzuia vifo vya takriban watu 92,000 kwa mwaka katika mabara hayo, vifo ambavyo vingetokana na ulaji mwingi wa chumvi. Kwa mfano, utafiti uliofanywa mwaka 2012 na Dk Derin Balogun anayeongoza kampeni ya kuzuia maradhi ya moyo na shinikizo la damu duniani, ulibainisha kwamba, hoteli nyingi za Waafrika na watu weusi jijini London, Uingereza, hupika vyakula vyenye chumvi nyingi zaidi. Kwa mujibu wa Dk. Balogun, gramu 12 zilipatikana katika wali na maharagwe, gramu 8.6 ndani ya wali maarufu kwa jina la 'Jollof' kutoka Afrika Magharibi, wakati gramu 19 iligundulika kwenye mikate. Hii ni chumvi zaidi ya gramu tano, zinazotakiwa kwa mtu mzima kutumia kila siku. Si vibaya ukifahamu kwamba chumvi ya asili hupatikana pia ndani ya vyakula vya asili vyenye madini ya Sodium kama vile mayai, nyama na hata baadhi ya vyakula vinavyotokana na maziwa. Mayai kwa mfano, yana miligramu 30 za Sodium. Kwa wale wanaopendelea kula vyakula vinavyopikwa nje ya nyumba zao, kama vile katika hoteli na kwenye migahawa, wanapaswa kuwa waangalifu mno kwa kuwa vyakula vya ‘fast food’ ni vyenye kiwango kikubwa cha chumvi na mafuta pia. Vyakula kama vile chizi, soseji, sosi ya soya na achari mbalimbali ni vyenye kutengenezwa kwa kutumia kiwango kikubwa cha chumvi. Lakini pia chumvi hutumiwa katika kuhifadhi baadhi ya vyakula vya makopo na maboksi. Elimu kama hii ya faida na madhara ya chumvi ni muhimu kwa Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuipatia kipaumbele kwa kutoa kwa wananchi wake, kwa faida ya taifa na watu wake. Ipo haja kwa jamii nzima ya Watanzania kuelimishwa vya kutosha kuhusu faida na madhara ya chumvi katika mwili mwa mwanadamu kuliko ilivyo sasa ambapo wananchi wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu ulaji wa chumvi.

No comments: