
WASICHANA wanaopata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18 pamoja na wenye tabia ya kutoa mimba mara kwa mara, wametajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Mbali na kundi hilo, pia watumiaji wa dawa za kulevya, watu wenye magonjwa ya zinaa, wanawake wanaozaa mara kwa mara na wanaume wasio tahiriwa nao wapo katika hatari ya kupata aina hiyo ya saratani.
Mshauri wa masuala ya Afya ya Uzazi, Leojin Mnzava, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibaha, amebainisha hayo katika mafunzo ya kuwapatia elimu hiyo ya Afya ya Uzazi wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wilayani humo na kuwa tayari wameanza kutoa elimu ya ugonjwa wa Saratani ya shingo ya kizazi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanafunzi walio na tabia ya kufanya mapenzi kabla ya wakati.
Amesema kwamba saratani ya shingo ya kizazi, ni hatari kuliko magonjwa mengine kama vile Ukimwi na Malaria, hivyo wanawake wanapaswa kuwa makini na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha au kuchochea magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa huo.
Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Asasi ya Maendeleo ya Wanawake ya INUKA, Gaudience Msuya, yenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam, amesema wametoa mafunzo kwa walimu 40 waliopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, ambayo yamelenga kuwakumbusha walimu visababishi vya saratani ya shingo ya kizazi ili waielimishe jamii wakiwemo wanafunzi.
Lindi yatajwa kuongoza Saratani za Matiti na Shingo ya kizazi
Wakati huo huo, Mkoa wa Lindi umetajwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake waliogundulika kuwa na saratani ya matiti na shingo ya kizazi kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutambua dalili za ugonjwa huo, ambao kama ukitambuliwa mapema unatibika.
Daktari Faridi Ally kutoka Hospitali ya Sokoine iliyoko Mkoani Lindi, amebainisha hayo wakati wa mahojiano na FikraPevu na kwamba wataalamu kutoka katika hospitali hiyo wamekwishaanza kutoa elimu kwa wanawake zaidi ya 300, juu ya kutambua dalili za ugonjwa wa saratani na kusisitiza umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo.
Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza, amesema mipango ya Serikali ya mkoa ni pamoja na kuwa na kitengo maalumu cha kutibu maradhi hayo na kwamba kwa kuanza wameanza kutoa elimu ili kupunguza tatizo kabla ya mipango hiyo haijakamilika.
Saratani ya kizazi ni nini?
Ni aina ya saratani inayoshambulia seli/chembechembe zilizoko kwenye ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi. Chanzo cha ugonjwa huo ni kirusi kiitwacho 'Human Pailloma Virus' na huambukizwa kwa njia ya kujamiana na mtu mwenye maambukizi hayo.
Aidha, dalili za ugonjwa ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na majimaji au uchafu usio wa kawaida ukeni, kutokwa na damu ukeni wakati ambao mwanamke hayuko kwenye hedhi pamoja na maumivu makali wakati wa kujamiana.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi za Afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) zimebainisha kwamba tabia hatarishi inayopelekea kupata magonjwa haya ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 18), uvutaji wa sigara, kuzaa mara kwa mara, matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula, kuwa na wapenzi wengi au kujamiana na mtu mwenye wapenzi wengi.
No comments:
Post a Comment